Ligi Kuu ya NBC iliendelea leo ambapo mechi zilipigwa mkoani Arusha na kule Manyara.
Mchezo uliokuwa ukifuatiliwa kwa karibu na mashabiki wa soka nchini ni kati ya TRA United dhidi ya Simba uliopigwa uwanja wa Shelkh Amri Abeid.
Dakika 90 za mchezo huo zimemalizika kwa matokeo ya suluhu ya bila kufungana huku TRA United wakijilaumu kwa kushindwa kuondoka na alama zote tatu.
TRA United walikuwa bora zaidi wakitengeneza mashambulizi ya hatari zaidi huku winga Ramadhan Chobwedo akiwapa wakati mgumu walinzi wa Simba.
Matokeo hayo ni wazi yamewasononesha mashabiki wa Simba kwani walihitaji kuona timu yao inaibuka na ushindi ili kuendelea kuwapa presha watani zao Yanga kwenye mbio za ubingwa.
Simba sasa iko nyuma ya Yanga kwa tofauti ya alama nane baad ya kufikisha alama 36 huku Yanga ikiongoza ligi na alama 44, Simba ikiwa na mechi moja ya kiporo pia.
Katika mchezo mwingine uliopigwa Manyara, Mbeya City imeiwekea ngumu Azam Fc ikilazimisha suluhu ya bila kufungana.
Hiyo ni sare ya 10 kwa Azam Fc msiimu huu matokeo ambayo yanazidi kufifisha matumaini yao ya kuwania ubingwa kwani sasa wako nyuma ya vinara Yanga kwa tofauti ya alama 10.



