Shamra shamra za ubingwa Arsenal usipime

Joel JJ By Joel JJ • 20th May 2026


Shamra shamra za ubingwa Arsenal usipime

Mashabiki wa Arsenal FC wameingia kwenye historia mpya baada ya klabu hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England kwa mara ya kwanza ndani ya miaka 22, jambo lililosababisha shamrashamra kubwa ndani na nje ya jiji la London.

Ubingwa huo ulithibitishwa baada ya Manchester City FC kushindwa kupata ushindi dhidi ya AFC Bournemouth kwa kutoka sare ya bao 1-1, matokeo yaliyoifanya Arsenal kuongoza ligi kwa tofauti ya alama nne ambayo haiwezi kufikiwa tena ukiwa umesalia mchezo mmoja kuhitimisha msimu.

Emirates yafurika mashabiki

Mara tu baada ya kipenga cha mwisho, maelfu ya mashabiki wa Arsenal walimiminika nje ya Emirates Stadium kusherehekea mafanikio hayo makubwa. Nyimbo, fataki, bendera na sare nyekundu na nyeupe vilitawala mitaa ya North London huku mashabiki wakionyesha furaha yao baada ya kusubiri kwa zaidi ya miongo miwili.

Katika baadhi ya maeneo maarufu ya mashabiki wa Arsenal kama baa za karibu na Emirates, mashabiki walionekana wakilia kwa furaha, kuimba nyimbo za klabu na kufanya maandamano ya usiku mzima wakiamini huu ni mwanzo wa zama mpya chini ya kocha Mikel Arteta.

Wachezaji wafanya sherehe hadi alfajiri

Ripoti kutoka England zinaeleza kuwa wachezaji wa Arsenal walikusanyika katika kituo cha mazoezi kushuhudia mchezo wa Manchester City kabla ya kuanza sherehe kubwa mara baada ya matokeo kuthibitisha ubingwa wao. Baadhi yao walionekana katika Emirates Stadium majira ya saa 11 alfajiri wakiendelea na shamrashamra hizo.

Nyota wa timu hiyo akiwemo Declan Rice, Bukayo Saka na nahodha Martin Ødegaard walichapisha picha na video mbalimbali mitandaoni wakionyesha furaha yao ya kutwaa taji hilo lililokuwa limewasumbua kwa miaka mingi.

Ian Wright na mastaa wa zamani wajitokeza

Miongoni mwa walioungana na mashabiki kusherehekea ni nguli wa Arsenal Ian Wright ambaye alionekana nje ya Emirates akiimba na kucheza pamoja na mashabiki wa klabu hiyo.

Pia viongozi mbalimbali nchini England walitoa pongezi zao, akiwemo Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer ambaye ni shabiki wa Arsenal.

Arteta aandika historia mpya

Ubingwa huo unatajwa kuwa mafanikio makubwa kwa Mikel Arteta ambaye amekuwa akiijenga Arsenal kwa miaka kadhaa baada ya vipindi vya misimu ya kukaribia ubingwa bila mafanikio. Arsenal sasa imefikisha mataji 14 ya ligi kuu ya England na kuvunja ukame uliodumu tangu zama za kikosi maarufu cha “Invincibles” mwaka 2004.

Mashabiki wengi wanaamini mafanikio hayo yanaweza kuwa mwanzo wa enzi mpya ya mafanikio kwa klabu hiyo ambayo pia bado ina nafasi ya kutwaa taji la Ulaya msimu huu.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.