Klabu ya Simba SC imetangaza azma ya kupeleka shauri lake katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Michezo,Court of Arbitration for Sport (CAS), kufuatia kutoridhishwa na uamuzi wa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Tanzania Football Federation uliotupilia mbali kesi yao dhidi ya mchezaji Mohamed Damaro.
Hatua hiyo imetangazwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba,Crescentius Magori, aliyesema klabu hiyo imefanya tathmini ya kina na kubaini kuwa kuna dosari katika maamuzi yaliyotolewa na mamlaka husika.
Magori alisema mbali na kwenda CAS, Simba pia inapanga kuiandikia barua FIFA kupinga hatua ya kumpa uraia wa Tanzania mchezaji huyo, wakidai hana sifa za kuitumikia timu ya Taifa.
Alieleza kuwa suala hilo linaibua maswali kuhusu usawa wa kanuni katika uendeshaji wa soka nchini, akidai kuwa linaweza kuipa faida klabu moja kwa kuwa na wachezaji wa kigeni zaidi ya kiwango kinachoruhusiwa.
“Kuhusu mchezaji Mohamed Damaro, tulikaa na kutafakari kwa kina, ni jambo ambalo halijakaa sawa. Ni kama kuna klabu moja inatumia nafasi hiyo kuwa na wachezaji wa kigeni zaidi ya walioruhusiwa kikanuni,” alisema Magori.
Aidha, alibainisha kuwa mwaka jana Simba iliwasilisha maombi ya kubadili uraia kwa baadhi ya wachezaji wake, lakini hadi sasa hayajajibiwa, jambo alilodai linaonyesha kukosekana kwa mizania sawa kwa klabu zote.
“Mwaka jana na sisi tuliandika barua ya kubadili uraia wa wachezaji wetu lakini haijajibiwa hadi leo. Ligi ikiwa haina mizania sawa si jambo linalokubalika,” alisisitiza.
Magori aliongeza kuwa si sahihi kwa mchezaji kupewa uraia kwa lengo la kuchezea klabu pekee bila kuwa na uwezo wa kuitumikia timu ya Taifa.
“Kama mtu anapewa uraia ili tu achezee klabu bila timu ya taifa si jambo linalokubalika. Damaro hata ipite miaka 100 hawezi kucheza timu ya Taifa,” alisema.



