Baada ya sintofahamu ya wiki kadhaa, inaelezwa klabu ya Singida Black Stars na mshambuliaji wake wa kimataifa kutoka Kenya, Elvis Rupia, wamefikia makubaliano ya pande mbili kusitisha mkataba.
Hatua hii inakuja ikiwa ni mwendelezo wa taarifa zilizokuwa zikisambaa awali, zikieleza kuwa Rupia alijiondoa kambini kutokana na madai mbalimbali kwa uongozi wa Singida BS.
Awali, Rupia aliondoka katika mazingira yaliyozua maswali kwa mashabiki wa Singida BS, akiwa hajaonekana kwenye kikosi cha timu hiyo kwa wiki kadhaa.
Inadaiwa kuwa chanzo kikuu cha sintofahamu hiyo kilikuwa ni madai ya stahiki mbalimbali kulingana na makubaliano ya kimkataba baina yake na Singida BS.
Rupia ameichezea Singida Black Stars kwa takribani misimu mitatu, akiwa miongoni mwa washambuliaji waliotoa mchango mkubwa katika safu ya ushambuliaji ya timu hiyo. Sasa yuko huru kujiunga na klabu nyingine katika dirisha lijalo la usajili litakalofunguliwa baada ya msimu huu kufika tamati.



