Robo fainali CRDB Cup; Simba yapewa TRA United, Wananchi wapelekwa JKT Tanzania

Joel JJ By Joel JJ β€’ 17th April 2026


Robo fainali CRDB Cup; Simba yapewa TRA United, Wananchi wapelekwa JKT Tanzania

Ratiba ya hatua ya robo fainali ya CRDB Federation Cup 2025/26 imetangazwa rasmi baada ya droo kufanyika leo jijini Dar es salaam.

Kwa mujibu wa droo hiyo, Yanga watamenyana na JKT Tanzania katika pambano linalotarajiwa kuwa na ushindani mkali, JKT Tanzania wakiwa wenyeji dimba la Isamuhyo.

Yanga haijawahi kupata ushindi katika mechi zote walizocheza dhidi ya JKT Tanzania dimba la Isamuhyo, hivyo wakati huu watakuwa na kazi ya kusaka ushindi wao wa kwanza mbele ya maafande hao katika uwanja wao. Ikumbukwe pia Yanga bado hawajamaliza na JKT Tanzania kwenye mchezo wa ligi duru ya pili ambao pia utapigwa Isamuhyo

Katika mchezo mwingine, Simba SC watakutana na TRA United FC, huku Wekundu wa Msimbazi wakisaka tiketi ya kusonga mbele dhidi ya wapinzani wao wanaokuja kwa kasi katika soka la Tanzania. Mchezo huo pia utapigwa uwanja wa Isamuhyo Simba wakiwa wenyeji.

Nayo Coastal Union itakuwa wenyeji wa Singida Black Stars katika mchezo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkali ukipigwa uwanja wa Mkwakwani mkoani Tanga.

Kwa upande mwingine, Mashujaa FC itawakaribisha Azam FC mkoani Kigoma, mchezo mwingine ambao unatarajiwa kuwa na upinzani mkali. Mashujaa Fc tayari wamekutana na Aza Fc mara moja kwenye mchezo wa ligi kuu uliopigwa uwanja wa Lake Tanganyika na kumalizika kwa suluhu ya bila kufungana.

Wakati huu watakutana katika mchezo ambao lazima mshindi apatikane kuelekea hatua ya nusu fainali.

Droo hiyo pia imebainisha mwelekeo wa nusu fainali, ambapo mshindi kati ya Simba na TRA United atakutana na mshindi wa Coastal Union dhidi ya Singida Black Stars. Aidha, mshindi wa mchezo kati ya Mashujaa na Azam Fc atamenyana na mshindi wa pambano kati ya JKT Tanzania na Yanga.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.