Kocha wa zamani wa klabu ya CR Belouizdad, Sead Ramovic, ameripotiwa kuwasilisha malalamiko katika shirikisho la soka duniani FIFA, kufuatia mgogoro wa kimkataba kati yake na klabu hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa nchini Algeria, Ramovic amechukua hatua hiyo baada ya kutokea mvutano unaohusiana na masuala ya utekelezaji wa mkataba wake, ikiwemo madai ya kucheleweshwa au kutotekelezwa kwa baadhi ya masharti ya kifedha.
Inaelezwa kocha huyo na nmaafisa wake katika benchi la ufundi wana madai ya malimbikizo ya mishahara kwa miezi minne.
Kocha huyo, ambaye amewahi pia kuinoa Young Africans SC kabla ya kuhamia Algeria, pia anadaiwa kuwa katika mgogoro wa kiuongozi uliodumu kwa muda na uongozi wa CR Belouizdad.
Ramovic alitua Belouizdad msimu uliopita baada ya kuachana na Yanga ambapo katika msimu mmoja alioinoa timu hiyo, mafanikio makubwa ni kuwafikisha nusu fainali ya kombe la Shirikisho (CAFCC) msimu huu.
Hata hivyo hakushuhudia mechi za nusu fainali kwani tayari uongozi wa Belouizdad ulikuwa umemsimamisha kabla ya kutangaza kumfuta kazi hivi karibuni.



