Winga wa Barcelona na timu ya taifa ya Brazil, Raphinha, ameripotiwa kuwa tayari kwa mchezo mkubwa wa El Clásico dhidi ya Real Madrid, baada ya kurejea kutoka kwenye majeraha yaliyomweka nje kwa muda.
Kwa mujibu wa taarifa za hivi karibuni, Raphinha ameonesha dalili nzuri za kupona na yuko kwenye mipango ya kikosi cha Barcelona kuelekea mchezo huo muhimu wa La Liga utakaopigwa Jumapili, May 06.
Kocha wa Barcelona, Hansi Flick, ameripotiwa kuwa na mpango maalum wa kumtumia Raphinha kwa dakika chache za mwisho au kumjumuisha kikosini kulingana na hali yake ya utimamu wa mwili, huku akipanga kwa makini safu ya ushambuliaji kutokana na ushindani mkubwa ndani ya kikosi.
Raphinha amekuwa mmoja wa wachezaji muhimu wa Barcelona msimu huu, akichangia mabao na pasi za mwisho katika michezo muhimu, ikiwemo ushindi dhidi ya Real Madrid kwenye baadhi ya mechi zilizopita ambapo alionesha kiwango cha juu cha ufungaji na ubunifu wa hali ya juu .
Hata hivyo, mchezaji huyo amekuwa akisumbuliwa na majeraha ya misuli (hamstring) yaliyomfanya kukosa baadhi ya michezo muhimu ya klabu na timu ya taifa.
Licha ya changamoto hizo, ripoti zinaonesha kuwa kurejea kwake kunachukuliwa kama nyongeza muhimu kwa Barcelona katika mchezo huo wa kihistoria ambao unaweza kuwapa taji la La Liga kwa msimu wa pili mfululizo.



