Rais wa klabu ya Florentino Pérez amezungumzia kwa nguvu sera yake ya usajili wa wachezaji nyota, akisisitiza azma yake ya kuendelea kujenga kikosi chenye mastaa wa kiwango cha dunia kuelekea kipindi kipya cha uongozi.
Katika kauli yake inayohusishwa na kampeni ya kuwania nafasi ya uongozi ndani ya klabu, Pérez ameahidi kuwa Real Madrid ipo tayari kufanya usajili mkubwa wa euro milioni 150, akieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya kuendeleza falsafa yake ya “Galácticos” iliyoijenga historia ya mafanikio ya klabu hiyo.
“Nimemsajili Zidane, Figo, Beckham, Cristiano Ronaldo au Kaká... mchezaji wa €150m ni Galactico. Mchezaji tutakayemuwania yuko katika kategoria hiyo hiyo,” alinukuliwa akisema, akisisitiza mwelekeo wake wa kuendeleza sera hiyo kama alivyofanya miaka ya nyuma.
Kauli hiyo imekuja katika kipindi ambacho Real Madrid inaendelea kujiandaa kwa mustakabali mpya baada ya kumaliza msimu bila taji lolote.
Pérez ameendelea kusisitiza kwamba dira yake ya uongozi inabaki ile ile ya kuleta wachezaji bora duniani ndani ya Santiago Bernabéu ili kuimarisha ushindani wa klabu hiyo Ulaya.
Pia amezungumzia mipango ya kiufundi akihusisha usajili na mabadiliko ya kikosi, akitaja uwezekano wa kuimarishwa kwa baadhi ya maeneo ya timu kuelekea msimu ujao.



