Okello anukia ligi kuu ya Uturuki

Joel JJ By Joel JJ β€’ 12th May 2026


Okello anukia ligi kuu ya Uturuki

Maafisa wa klabu ya Uturuki, Fenerbahce S.K., wameripotiwa kuwepo nchini Tanzania kwa muda wa siku nne wakimfuatilia kiungo mshambuliaji wa Young Africans S.C, Allan Okello.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa mwanahabari wa Uganda, Ronnie Santos Mwine, wageni hao kutoka Uturuki wamevutiwa na kiwango cha mchezaji huyo wa kimataifa wa Uganda ambaye ameonyesha makali tangu ajiunge na Yanga katika dirisha dogo la usajili.

Okello ameanza maisha yake mapya kwa kishindo, akiwa tayari amechangia mabao matano na kutoa pasi za mabao saba kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, jambo lililomfanya kuwa miongoni mwa wachezaji wanaofuatiliwa kwa karibu.

Inaelezwa kuwa maafisa wa Fenerbahce wanatarajiwa kuwepo uwanjani kesho wakati Yanga itakapovaana na Dodoma Jiji FC katika mchezo wa ligi utakaopigwa kwenye Uwanja wa Airtel Mtipa mkoani Singida.

Iwapo klabu hiyo ya Uturuki itaamua kumsajili Okello, itawalazimu kufungua mazungumzo rasmi na Yanga, ingawa hadi sasa hakuna mazungunzo yaliyoanza kati ya pande hizo mbili.

Okello alijiunga na Yanga akitokea Vipers SC ya Uganda, akisaini mkataba wa miaka miwili na nusu, na sasa anaendelea kuonyesha mchango mkubwa katika kikosi hicho cha Jangwani.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.