Mvutano mkubwa unatarajiwa kushuhudiwa kwenye dirisha lijalo la usajili kati ya wapinzani wa jadi wa soka Tanzania, Simba SC na Young Africans SC, huku wakianza mapema kupimana nguvu katika harakati za kumuwania mshambuliaji Suleiman Mwalimu.
Taarifa zinaeleza kuwa Yanga tayari imefungua mazungumzo na Wydad Athletic Club, kwa lengo la kuinasa saini ya mshambuliaji huyo ambaye kwa sasa anakipiga Simba kwa mkopo. Mkataba wake wa mkopo unatarajiwa kumalizika mwezi Juni, ambapo atalazimika kurejea kwa waajiri wake wa kudumu.
Yanga inaonekana kuwa na mpango mkakati wa kuimarisha safu yao ya ushambuliaji kuelekea mashindano ya kimataifa ya CAF Champions League msimu ujao. Ndani ya kikosi hicho, utegemezi mkubwa kwa sasa uko kwa washambuliaji Depu na Prince Dube, hali inayowafanya viongozi kuona umuhimu wa kuongeza nguvu mpya yenye ushindani.
Faida kubwa kwa Yanga ni kwamba Mwalimu ni mchezaji wa ndani hivyo kama watafanikiwa kumsajili, watakuwa wameongeza uwiano mzuri wa kikosi bila kuathiri nafasi za wachezaji wa kigeni.
Hata hivyo, Simba hawapo tayari kumuachia kirahisi. Uongozi wa klabu hiyo una mpango wa kuhakikisha wanambakisha mshambuliaji huyo ambaye amekuwa tegemeo muhimu katika kikosi chao msimu huu. Mwalimu anaongoza kwa mabao ndani ya Simba akiwa tayari amefunga sita, akionyesha uthabiti mkubwa katika safu ya ushambuliaji.
Kuongezeka kwa umuhimu wake kumekuja hasa baada ya mshambuliaji Jonathan Sowah kusimamishwa kwa tuhuma za utovu wa nidhamu, hali iliyomlazimu kutolewa kwenye kikosi cha kwanza na hivi karibuni Simba ikitangaza kumuagiza akafanye mazoezi na timu ya vijana.



