Mwalimu aipeleka Simba robo fainali kombe la CRDB, Singida BS, TRA United nazo zafuzu

Joel JJ By Joel JJ β€’ 12th April 2026


Mwalimu aipeleka Simba robo fainali kombe la CRDB, Singida BS, TRA United nazo zafuzu

Klabu ya Simba SC imefanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya Kombe la CRDB baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Dodoma Jiji FC katika mchezo wa hatua ya 16 bora uliochezwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

Dodoma Jiji walikuwa wa kwanza kupata bao mapema dakika ya 9 kupitia kwa Khleffin Hamdoun, bao lililowapa matumaini ya kufanya vizuri kwenye mchezo huo. Hata hivyo, Simba walionyesha uthabiti na kurejea haraka mchezoni.

Mshambuliaji Suleiman Mwalimu aliisawazishia Simba dakika ya 54 kabla ya Anicet Oura kuongeza bao la pili dakika ya 60. Mwalimu alikamilisha ushindi huo kwa kufunga bao lake la pili na la tatu kwa Simba dakika ya 67 katika mchezo huo.

Kipindi cha pili kilishuhudia Simba wakicheza kwa udhibiti mkubwa vijana wa kocha Steve Barker, wakitumia vyema dakika 45 za kipindi hicho kuandikisha ushindi muhimu.

Ushindi huo unaipa Simba nafasi ya kusonga mbele katika michuano hiyo, ikiwa ni matokeo muhimu baada ya timu hiyo kutokuwa na mwenendo mzuri katika michezo yao miwili iliyopita.

Katika michezo mingine ya hatua hiyo, Singida Black Stars waliifunga Mbeya City FC mabao 5-1, huku TRA United ikiibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Namungo FC na kufuzu robo fainali.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.