Mudathir, Okello waimaliza Pamba Jiji

Joel JJ By Joel JJ β€’ 8th April 2026


Mudathir, Okello waimaliza Pamba Jiji

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya NBC, Yanga, wameendelea kuonesha ubora wao baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Pamba Jiji katika mchezo uliopigwa Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.

Katika mchezo huo, Yanga walidhibiti kwa kiasi kikubwa umiliki wa mpira na kutengeneza nafasi nyingi za kufunga. Kiungo Mudathir Yahya alikuwa nyota wa mchezo baada ya kufunga mabao mawili katika dakika ya 8 na 33, kabla ya Maxi Nzengeli kuongeza bao la tatu dakika ya 67 na kuhitimisha ushindi huo mnono.

Kiungo mshambuliaji Allan Okello alikuwa mwiba mkali kwa walinzi wa Pamba Jiji akitoa pasi za mabao yote matatu yaliyofungwa na Yanga.

Ushindi huo unaifanya Yanga kuendelea kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi wakifikisha alama 44 wakikaa kileleni kwa tofauti ya alama 9.

Kwa upande wa Pamba Jiji, walionekana kushindwa kuhimili kasi na ubora wa wapinzani wao, licha ya kucheza nyumbani mbele ya mashabiki wao.

Wakati huohuo, katika mchezo mwingine uliochezwa mapema, Singida Black Stars waliibuka na ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya KMC FC.

Mchezo huo ulikuwa na ushindani mkubwa, huku timu zote zikicheza kwa tahadhari. Singida BS walifanikiwa kupata bao pekee la ushindi lililofungwa la Lamine Jarjou kwenye dakika ya 70 na kuwapa alama tatu muhimu.

Singida BS na KMC ziliingia kwenye mchezo huo zikiwa kwenye presha kubwa ya kuhitaji matokeo zote zikiwa zimetimua makocha wao.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.