Kiungo mshambuliaji wa klabu ya Simba SC, Elie Mpanzu, ameendelea kuonyesha kiwango bora katika mechi za karibuni, akifunga mabao muhimu na kutoa pasi za mabao, huku akisisitiza azma yake ya kurejea katika kikosi cha kwanza.
Mpanzu, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, amejikuta akipoteza nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza kufuatia ujio wa washambuliaji wapya Anicet Oura na Libasse Gueye waliotua Msimbazi kupitia usajili wa dirisha dogo.
Hata hivyo, licha ya kukosa nafasi ya kudumu kikosini, Mpanzu ameendelea kutumia vyema dakika anazopewa na kocha Steve Barker, ambapo amekuwa miongoni mwa wachezaji wanaotoa mchango mkubwa kila anapoitwa uwanjani.
Kwa upande wao, Oura na Gueye nao wameonyesha ushindani mkali kwa nafasi za mbele baada ya wote kufunga mabao katika michezo ya hivi karibuni. Gueye amefunga mabao mawili katika mechi mbili zilizopita, wakati Oura naye akipachika mabao mawili katika mechi tatu za karibuni.
Oura pia alichaguliwa kuwa nyota wa mchezo katika ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Namungo FC, mchezo ambao alifunga bao moja muhimu lililosaidia timu yake kupata matokeo chanya.
Ushindani huo mkali ndani ya safu ya ushambuliaji ya Simba SC unatajwa kuwa chachu ya kuongeza ubora wa kikosi hicho, kwani wachezaji wote wanalazimika kuongeza juhudi ili kupata nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza.
Kocha Barker anakabiliwa na kazi ngumu ya kuchagua wachezaji kutokana na kiwango kizuri kinachoonyeshwa na washambuliaji wake wote, hali inayoongeza ushindani ndani ya timu na kuinufaisha Simba SC kwa ujumla katika mashindano mbalimbali.



