Mosimane atajwa timu ya Taifa Mali

Joel JJ By Joel JJ • 7th May 2026


Mosimane atajwa timu ya Taifa Mali

Kocha maarufu raia wa Afrika Kusini, Pitso Mosimane, ametajwa kuwa miongoni mwa makocha wanaopewa nafasi kubwa ya kuchukua wadhifa wa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Mali, kufuatia mchakato wa klabu hiyo kutafuta mrithi wa benchi la ufundi.

Kwa mujibu wa taarifa zilizonukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari vya michezo ikiwemo Koora, Mosimane amewekwa kwenye orodha fupi ya makocha watatu wanaoangaliwa kwa karibu, akiwemo Walid Regragui wa Morocco pamoja na Hervé Renard raia wa Ufaransa, wote wakiwa na uzoefu mkubwa katika soka la Afrika na kimataifa.

Majina hayo makubwa yamepewa kipaumbele kutokana na rekodi zao katika michuano mbalimbali ya bara la Afrika na Kombe la Dunia, ambapo kila mmoja ameonyesha uwezo wa kuiongoza timu katika viwango vya juu vya ushindani.

Mosimane kwa sasa hana klabu tangu alipoondoka Esteghlal ya Iran Januari 2025, hali inayoongeza uwezekano wa kurejea kazini kwa haraka endapo atapata ofa rasmi kutoka shirikisho la soka la Mali.

Kocha huyo anaheshimika sana barani Afrika kutokana na mafanikio yake akiwa na Mamelodi Sundowns pamoja na Al Ahly ya Misri, ambapo alifanikiwa kutwaa mataji mbalimbali ya ligi za ndani na michuano ya kimataifa, yakiwemo Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mafanikio yake hayo yameendelea kumuweka katika daraja la makocha wenye uzoefu mkubwa barani Afrika, jambo linaloifanya Mali kumwangalia kama mmoja wa wagombea wakuu wa nafasi hiyo nyeti.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.