Golikipa wa Singida Black Stars, Metacha Mnata ameomba radhi kufuatia tukio la kugomea kufanyiwa mabadiliko katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Young Africans SC uliochezwa uwanja wa KMC Complex juzi Singida BS wakikubali kipigo cha mabao 3-0.
Mnata alionekana kutokuwa tayari kutoka uwanjani muda mfupi baada ya kuruhusu bao kupitia mpira wa adhabu, kabla ya baadaye kukubali nafasi yake kuchukuliwa na golikipa mwingine wa timu hiyo, Abasogie Amos.
Kupitia ujumbe wake, Mnata amesema tukio hilo lilitokana na presha ya mchezo na hisia za ushindani, huku akisisitiza kuwa hakuwa na nia ya kuonyesha utovu wa nidhamu au kupuuza maamuzi ya benchi la ufundi.
“Naomba radhi kwa Mashabiki, Benchi la Ufundi, Viongozi na wapenzi wote wa Singida BS kutokana na sintofahamu iliyotokea kwenye mchezo wetu dhidi ya Young Africans SC.”
“Kilichotokea kilikuwa ni matokeo ya hisia za mchezo na presha ya ushindani, lakini haikuwa dhamira yangu kuonyesha utovu wa nidhamu wala kudharau maamuzi ya Benchi la Ufundi.”
“Ninaiheshimu timu yangu, kocha wangu na maamuzi yote yanayofanywa kwa maslahi ya klabu. Nimejifunza kutokana na tukio lile na nawaahidi nitaendelea kupambana kwa ajili ya timu kwa nidhamu, kujituma na mshikamano mkubwa zaidi na wenzangu,” alisema Metacha.
Baada ya kuomba radhi Singida BS haitarajiwi kumchukulia Metacha hatua zaidi.



