Mshambuliaji wa Pyramids FC, Fiston Mayele, aliibuka shujaa wa mchezo baada ya kufunga mabao mawili yaliyoipa timu yake ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Al Ahly katika mechi ya Ligi Kuu ya Misri iliyopigwa kwenye Uwanja wa 30 June jijini Cairo, Jumatatu usiku.
Baada ya kipindi cha kwanza kumalizika bila mabao, Pyramids walirejea kwa kasi kipindi cha pili wakionyesha dhamira ya kutwaa pointi zote tatu. Mayele alifungua ukurasa wa mabao dakika ya 70 kwa shuti lililomshinda kipa wa Al Ahly baada ya kugonga mchezaji na kubadilisha mwelekeo.
Mshambuliaji huyo raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo hakuishia hapo, kwani aliongeza bao la pili dakika ya 78 akimalizia vizuri shambulizi la kushtukiza, na kuwaacha mabeki wa Al Ahly wakiwa hawana majibu.
Katika dakika za nyongeza, Karim Hafez alifunga bao la tatu kwa mkwaju wa penalti, akihitimisha ushindi huo muhimu uliotikisa mbio za ubingwa wa ligi.
Ushindi huo umeipa Pyramids nguvu mpya katika kinyang’anyiro cha ubingwa, huku ukiiweka Al Ahly katika hali ngumu zaidi ya kufukuzia taji. Klabu hiyo yenye rekodi kubwa ya mafanikio barani Afrika sasa inakabiliwa na shinikizo kubwa la kushinda mechi zake zilizosalia ili kurejesha matumaini ya kutwaa ubingwa.



