Klabu ya Mbeya City imemteua Salum Mayanga kuwa kocha mkuu mpya kufuatia kuondoka kwa Mecky Maxime na benchi lake la ufundi. Uamuzi huu unakuja katika kipindi kigumu kwa timu hiyo, ambayo inapambana kujinasua kwenye hatari ya kushuka daraja.
Mayanga si mgeni ndani ya kikosi hicho cha “Wagonga Nyundo”. Aliwahi kuinoa timu hiyo zamani wakati ikishiriki Ligi ya Championship (daraja la kwanza), jambo linaloipa faida klabu kutokana na uzoefu wake na uelewa wa mazingira ya timu.
Hali ya Ligi Kuu ya NBC kwa Mbeya City si ya kuridhisha. Timu hiyo inashika nafasi ya 14 ikiwa na alama 17 baada ya michezo 19, nafasi inayoiweka karibu kabisa na mstari wa kushuka daraja. Presha ni kubwa, na macho yote sasa yanaelekezwa kwa Mayanga kuibadilisha hali hiyo kabla mambo hayajawa mabaya zaidi.
Mtihani wa kwanza kwa kocha huyo mpya utakuwa dhidi ya Mashujaa FC katika mchezo unaotarajiwa kuchezwa Alhamisi, Aprili 30, 2026. Mchezo huo utafanyika katika dimba la Tanzanite Kwaraa Stadium kuanzia saa 10:15 jioni.



