Klabu ya Manchester United imeongeza matumaini ya kumaliza katika nafasi za juu za Premier League baada ya ushindi muhimu wa mabao 2-1 dhidi ya Brentfordkatika mchezo uliopigwa Old Trafford Jumatatu usiku.
Ushindi huo umeifanya Manchester United kujiimarisha katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi, alama tatu mbele ya Liverpool hatua inayowaweka karibu zaidi kufuzu kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Mabao ya mapema yaamua mchezo
Katika mchezo huo, United walianza kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la kuongoza mapema kupitia kiungo mkongwe Casemiro, aliyefunga kwa kichwa dakika ya 11 kufuatia mpira wa kona.
Shinikizo liliendelea na kabla ya mapumziko mshambuliaji Benjamin Sesko aliongeza bao la pili dakika ya 37, akimalizia shambulizi la kushtukiza lililoanzishwa na nahodha Bruno Fernandes.
Brentford walijaribu kurejea mchezoni kipindi cha pili, lakini walifanikiwa kupata bao moja tu kupitia Mathias Jensen mwishoni mwa mchezo, huku United wakidhibiti ushindi huo hadi mwisho.
Matokeo hayo yameifanya Manchester United kufikisha pointi 61 na kubaki nafasi ya tatu, wakiwa mbele kwa pointi 11 dhidi ya nafasi ya sita huku michezo michache ikisalia.
Ushindi huo unawaweka katika nafasi nzuri sana ya kufuzu Ligi ya Mabingwa, huku ushindani wa nafasi nne za juu ukiendelea kupamba moto.
Kocha atoa tahadhari
Kocha wa muda Michael Carrick amesisitiza kuwa licha ya ushindi huo muhimu, bado timu inapaswa kuendelea kupambana hadi mwisho wa msimu.
Amesema mafanikio ya kufuzu michuano ya Ulaya hayapaswi kuwafanya wachezaji kuridhika mapema, akihimiza nidhamu na juhudi kuendelea katika mechi zilizosalia.



