Mabingwa wa Afrika, Mamelodi Sundowns, wameendelea kuonyesha ubora wao baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya RB Leipzig katika mechi ya kirafiki iliyochezwa usiku wa jana jijini Pretoria, Afrika Kusini.
Kikosi cha Leipzig, kinachoshiriki Bundesliga ya Ujerumani, kilikuwa cha kwanza kupata bao kupitia mshambuliaji kijana Samba Konaté aliyetikisa nyavu dakika ya 22 na kuwapa wageni uongozi wa 1-0 kabla ya mapumziko. Leipzig walionekana kutawala sehemu kubwa ya kipindi cha kwanza huku wakitengeneza nafasi kadhaa za hatari.
Hata hivyo, Mamelodi Sundowns walirejea kwa nguvu kipindi cha pili na kuonyesha kwa nini ni mabingwa wa Afrika. Baada ya kushindwa kutumia nafasi kadhaa za wazi mwanzoni mwa kipindi cha pili, wenyeji walifanikiwa kusawazisha kupitia Brayan León dakika ya 76 kufuatia pasi nzuri kutoka kwa Tashreeq Matthews.
Kadri mchezo ulivyoelekea ukingoni, Sundowns walizidi kuwashinikiza wageni wao. Brayan León alifunga bao lake la pili la mchezo dakika ya 89 na kugeuza matokeo kuwa 2-1, kabla ya Bennet Mokoena kuongeza bao la tatu katika dakika za nyongeza (90+2) na kuthibitisha ushindi mnono wa mabao 3-1 dhidi ya timu hiyo ya Bundesliga.



