Makocha Simba, Yanga wafunguka maandalizi ya Kariakoo Derby

Joel JJ By Joel JJ • 2nd May 2026


Makocha Simba, Yanga wafunguka maandalizi ya Kariakoo Derby

Msisimko wa dabi ya Kariakoo unazidi kupamba moto kuelekea pambano kali kati ya Simba SC na Yanga litakalopigwa Jumapili May 03 katika uwanja wa Isamuhyo.

Makocha wa timu zote mbili leo wakifunguka kuhusu maandalizi ya timu zao kuelekea mchezo huo mkubwa wa Ligi Kuu ya NBC.


Gonçalves: Tuko tayari kwa mpango tofauti

Kocha Mkuu wa Yanga, Pedro Gonçalves, amesema maandalizi ya kikosi chake yanaendelea vizuri na wamebakiza hatua za mwisho kabla ya mchezo wa Jumapili.

Ameeleza kuwa timu imepata siku tatu za maandalizi maalum na sasa wanakamilisha mikakati ya mwisho kuelekea pambano hilo muhimu.

“Tumekuwa na siku tatu za maandalizi kuelekea mchezo wa Jumapili. Huu ni mchezo wa ligi hivyo tumejiandaa na mpango tofauti,” alisema Gonçalves.

“Leo tutakuwa na maandalizi ya mwisho ya kimkakati. Tunasikitika hatukupata matokeo mazuri kwenye mchezo uliopita lakini naamini tuko katika njia sahihi.”

Kocha huyo ameongeza kuwa wanatarajia mchezo mgumu lakini wenye matokeo chanya kwa upande wao, huku akiwataka mashabiki kujitokeza kwa wingi kuisapoti timu.

“Tuna matumaini makubwa ya kufanya vizuri kesho. Mashabiki wetu waje kwa wingi kutuunga mkono. Hii ni nafasi muhimu kuongeza pengo la pointi.”

Gonçalves pia alizungumzia mchezo uliopita, akisema licha ya kutopata ushindi, aliridhishwa na kiwango cha wachezaji wake. Hata hivyo, alionesha kusikitishwa na kukosekana kwa kiungo Mudathir Yahya kutokana na adhabu ya kufungiwa, akilinganisha na hali ya mchezaji wa Simba aliyeonekana kutoadhibiwa kabla ya mchezo uliozikutanisha timu hizo March 1.

Hata hivyo, ameweka wazi kuwa Yanga haitategemea mchezaji mmoja na tayari kuna mbadala wa nafasi hiyo.


Barker: Tunahitaji ushindi ili kubaki kwenye mbio za ubingwa

Kwa upande wa Simba, kocha Steve Barker amesema mchezo wa kesho ni muhimu sana kwa mustakabali wa ubingwa wa msimu huu.

Akizungumza na waandishi wa habari, Barker alisisitiza kuwa kushinda Yanga ni lazima ikiwa Simba wanataka kuendelea kubaki kwenye mbio za taji.

“Kama tukipoteza mchezo dhidi ya Yanga, nafikiri matarajio ya ubingwa yatakuwa magumu zaidi,” alisema.

“Tunahitaji kushinda, hasa tukiwa uwanja wa nyumbani. Matokeo hayo yatatuweka katika nafasi nzuri.”

Ameongeza kuwa anatarajia mchezo mgumu lakini anaamini kikosi chake kiko tayari kupambana kwa nguvu zote, huku akiwataka mashabiki kujitokeza kwa wingi kuisapoti timu.

“Sisi ni Simba na tuko tayari kupambania kila alama,” alisisitiza Barker.


Simba na Yanga zinakutana katika mchezo huo muhimu wa ligi zikiwa zimepita takribani siku tano tangu timu hizo zilipokutana kwenye mchezo wa fainali kombe la Muungano Simba ikiibuka na ushindi katika mchezo huo uliopigwa kwa dakika 120.

Wakati huu timu hizo zinakutana huku kila moja ikihitaji alama tatu, Yanga wanaweza kujiweka katika nafasi nzuri ya kutetea ubingwa kama watashinda mchezo huo wakati Simba ushindi utaweka matumaini hai kwenye mbio za ubingwa kwani watapunguza gap la pointi kutoka tano hadi mbili lakini wakifungwa zitakuwa nane.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.