Makocha wa timu za Simba SC na Coastal Union wameanza kutambiana kuelekea mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaopigwa kesho Alhamisi Mei 21 katika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani mkali kutokana na umuhimu wake kwa kila upande, huku timu zote mbili zikiwa na malengo tofauti lakini muhimu katika msimamo wa ligi.
Barker: Tuko tayari, tunalenga pointi tatu
Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker, amesema kikosi chake kimekamilisha maandalizi na kiko tayari kwa pambano hilo, akisisitiza dhamira ya timu yake kushinda na kucheza soka safi.
Barker amesema Simba inaiheshimu Coastal Union, lakini imejiandaa vilivyo kuhakikisha inarudi na alama tatu muhimu.
Amesema:
“Tumekuwa na wakati mzuri wa kujiandaa na mchezo dhidi ya Coastal Union, tuko tayari. Tunamuheshimu mpinzani wetu lakini tutaingia kwenye mchezo wa kesho kuonyesha ubora wetu.”
“Kulingana na maandalizi mazuri tuliyofanya kuelekea mchezo huu, naamini tunakwenda kupata ushindi,” alisema Barker.
Kocha huyo ameongeza kuwa ushindi katika mchezo huo unaweza kuisaidia Simba kupanda kileleni mwa msimamo wa ligi, hatua ambayo itaongeza presha katika mbio za ubingwa wa msimu huu.

Fikiri Elias: Tutawapa Simba mtihani mgumu
Kwa upande wake, kocha wa Coastal Union, Fikiri Elias, amesema timu yake imejipanga kutoa upinzani mkali na kuhakikisha inapata matokeo chanya dhidi ya Simba.
Elias amesema Coastal Union haitakuwa uwanjani kama daraja la kuwapandisha wapinzani, bali itapigania pointi tatu kwa nguvu zote.
Amesema:
“Tumejiandaa kuwapa changamoto kubwa Simba uwanjani, lazima tuulize maswali magumu ya kimbinu dakika 90.”
“Hatutaki kuwa daraja la kumnyanyua yoyote, lazima tutafute alama tatu kwa ajili ya timu yetu na kujiweka nafasi nzuri zaidi.”
“Kila mchezo una ladha yake, tumejiandaa vizuri kucheza dakika 90 kwa kumpa heshima mpinzani wetu. Pia eneo ambalo tupo kwenye msimamo wa ligi kuu linatupa morali kubwa ya kupambana na kutafuta alama tatu.”
Mchezo wa presha na malengo tofauti
Mchezo huu unatarajiwa kuwa mgumu kutokana na Simba kutafuta ushindi ili kuendeleza ushindani wa ubingwa, huku Coastal Union ikipambana kuboresha nafasi yake kwenye msimamo wa ligi.
Mashabiki wa pande zote mbili wanatarajiwa kujitokeza kwa wingi Mkwakwani kushuhudia pambano hilo la kusisimua la Ligi Kuu Tanzania Bara.



