Beki wa kati wa kimataifa wa Ufaransa, Ibrahima Konaté, ameripotiwa kufikia makubaliano ya awali kujiunga na miamba wa Hispania, Real Madrid, katika mkataba wa miaka minne kama mchezaji huru.
Kwa mujibu wa taarifa, Konaté ameondoka rasmi katika klabu ya Liverpool FC baada ya mkataba wake kumalizika, na amechagua kuanza ukurasa mpya katika dimba la Santiago Bernabéu.
Inaelezwa kuwa hatua ya kukamilika kwa dili hilo bado inategemea baadhi ya vigezo vya ndani ya klabu ya Real Madrid, ikiwemo mchakato wa kisiasa wa ndani unaohusishwa na uwezekano wa kuchaguliwa tena kwa rais wa klabu, Florentino Pérez.
Aidha, ripoti zinaeleza kuwa kocha ajaye wa klabu hiyo, José Mourinho, pamoja na nyota wa Ufaransa, Kylian Mbappé, wanatajwa kuwa miongoni mwa watu wanaoshinikiza uhamisho huo ukamilike haraka kutokana na kuamini uwezo wa Konaté kuimarisha safu ya ulinzi.
Konaté, ambaye amekuwa mmoja wa mabeki imara zaidi katika soka la Ulaya katika miaka ya hivi karibuni, anatarajiwa kuongeza nguvu kubwa katika safu ya ulinzi ya Real Madrid ikiwa dili hilo litakamilika rasmi kama inavyoripotiwa.
Katika kipindi chake Liverpool, beki huyo amejijengea heshima kubwa kutokana na uimara wake, kasi na uwezo wa kuongoza safu ya nyuma, akichangia mafanikio ya klabu hiyo katika mashindano mbalimbali ya ndani na Ulaya.



