Mabingwa watetezi wa Kombe la Dunia, Argentina, wanaingia kwenye michuano ya Kombe la Dunia 2026 wakiwa na matumaini makubwa ya kutetea taji lao walilotwaa nchini Qatar mwaka 2022 baada ya kuifunga Ufaransa katika fainali iliyosisimua dunia ya soka.
Argentina ilitwaa ubingwa huo kwa ushindi wa penalti 4-2 baada ya sare ya mabao 3-3 ndani ya dakika 120 za mchezo uliochezwa katika Uwanja wa Lusail, Qatar. Nahodha wao, Lionel Messi, aliandika historia kwa kunyanyua kombe hilo kwa mara ya kwanza katika maisha yake ya soka ya kimataifa.
Argentina yapangwa Kundi J
Katika michuano ya mwaka huu, Argentina imepangwa Kundi J pamoja na mataifa yafuatayo:
- Algeria
- Austria
- Jordan
Wachambuzi wa soka wanaiona Argentina kuwa timu yenye nafasi kubwa ya kuongoza kundi hilo kutokana na uzoefu na ubora wa kikosi chake.
Ratiba ya Michezo ya Argentina
| Mchezo | Tarehe |
|---|---|
| Argentina vs Algeria | Juni 17, 2026 |
| Argentina vs Austria | Juni 22, 2026 |
| Jordan vs Argentina | Juni 28, 2026 |
Messi bado gumzo
Swali kubwa linaloulizwa na mashabiki duniani kote ni kama Lionel Messi ataendelea kuichezea Argentina katika michuano hiyo. Messi ana umri wa miaka 39 lakini bado hajathibitisha rasmi kustaafu kuitumikia timu ya taifa ingawa kama atashiriki michuano ya mwaka huu basi huenda akastaafu baada ya michuano hiyo.
Wengi wanaamini kuwa uzoefu wake utaendelea kuwa silaha muhimu kwa Argentina huku nyota wengine kama Julián Álvarez, Enzo Fernández na Alexis Mac Allister wakitarajiwa kubeba majukumu makubwa zaidi.
Mataifa yanayopewa nafasi kutwaa Ubingwa
- Argentina
- Ufaransa
- Brazil
- England
- Spain
- Portugal
Mashindano ya mwaka huu yatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa zaidi kutokana na kuongezeka kwa idadi ya timu (48) pamoja na mfumo mpya wa michuano.
Kombe la Dunia la kihistoria
Tofauti na miaka iliyopita, Kombe la Dunia 2026 litakuwa na jumla ya mechi 104 huku mataifa mengi zaidi yakipata nafasi ya kushiriki hatua ya mtoano.



