Kocha Mkuu wa Yanga, Pedro Goncalves, amesema kikosi chake kiko tayari kwa mtanange mgumu wa nusu fainali ya Kombe la Muungano dhidi ya Azam FC utakaopigwa Jumamosi katika Uwanja wa New Amaan Complex.
Akizungumza na waandishi wa habari visiwani Zanzibar, Goncalves alisema licha ya muda mfupi wa maandalizi, kikosi chake kimejiandaa vyema kwa ajili ya mchezo huo muhimu, akisisitiza kuwa wanatarajia ushindani mkali.
Alisema Azam FC ni miongoni mwa timu bora na imekuwa ikipeleka upinzani mkubwa kila wanapokutana, hali inayoongeza uzito wa pambano hilo.
“Tunatarajia kuwa na mchezo mgumu na wa ushindani mkubwa kwa sababu tunakutana na timu yenye ubora. Kila mara tunapocheza na Azam FC huwa wanatupa upinzani mkali,” alisema Goncalves.
Aliongeza kuwa pamoja na ratiba kuwa ngumu kutokana na ukaribu wa mechi kwenye michuano hiyo pamoja na ligi, kikosi chake kimefanya maandalizi kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha kinafikia malengo ya kutinga fainali.
Yanga, ambao ni mabingwa watetezi wa michuano hiyo, wanalisaka taji hilo kwa msimu wa pili mfululizo, ushindi utawathibitishia kuandikisha fainali yao ya pili mtawalia.
Mshindi wa mchezo huo atasonga mbele kusubiri mshindi wa nusu fainali nyingine kati ya Mlandege FC na Simba SC, ambao watakutana Jumapili.



