Kocha Mkuu wa Young Africans SC, Pedro Goncalves amesema kikosi chake kiko tayari kikamilifu kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Mbeya City FC, huku akisisitiza kuwa lengo lao kuu ni kupata alama zote tatu.
Akizungumza kuelekea mchezo huo utakaopigwa Alhamisi, Aprili 16 katika uwanja wa KMC Complex, Goncalves alikiri kuwa hautakuwa mchezo rahisi, lakini ana imani kubwa na uwezo wa kikosi chake kufanya vizuri.
"Tunatambua ugumu wa mchezo huu, lakini tupo tayari kupambana. Kikosi changu kipo kwenye hali nzuri na tunahitaji alama tatu ili kuendelea kujiweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi," alisema Goncalves.
Kocha huyo pia alieleza kuwa katika mchezo uliopita alifanya mabadiliko kadhaa kwa makusudi, ili kuwapa nafasi baadhi ya wachezaji kupata utimamu wa mwili pamoja na kupumzisha nyota wake muhimu, jambo analoamini litazaa matunda katika mchezo ujao.
Habari njema kwa upande wa Yanga ni kurejea kwa mshambuliaji Prince Dube ambaye alikuwa nje kutokana na majeraha. Goncalves anaamini uwepo wake utaongeza nguvu na ufanisi katika safu ya ushambuliaji.
"Nina matarajio makubwa baada ya kurejea kwa Dube. Tayari alianza kupata dakika chache kwenye mchezo uliopita na ninaamini ataongeza makali zaidi katika ushambuliaji wetu," aliongeza.
Hata hivyo, Goncalves alisisitiza umuhimu wa tahadhari dhidi ya wapinzani wao Mbeya City FC, akibainisha kuwa wana kikosi kizuri chenye uzoefu na wanaweza kuwa hatari.
"Lazima tuwaheshimu wapinzani wetu. Mbeya City wana kikosi kizuri na uzoefu mkubwa. Umakini ni muhimu kwa sababu mpira ni mchezo wa makosa, kosa moja linaweza kuamua matokeo," alisisitiza.
Pamoja na kurejea kwa Dube, kocha huyo alikiri bado kuna changamoto ya majeraha kwa baadhi ya wachezaji, hali inayolazimisha benchi la ufundi kutafuta mbinu mbadala ya kuziba mapengo yaliyopo.
Kwa ujumla, Young Africans SC inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na morali ya juu, ikilenga kuendelea kulinda nafasi yake kileleni mwa msimamo wa ligi huku mashabiki wakitarajia ushindi na burudani uwanjani.



