Kikosi cha Simba SC kimepania kufuzu hatua ya fainali ya Kombe la Muungano baada ya kocha mkuu Steve Barker kueleza wazi kuwa lengo lao ni kupata ushindi dhidi ya Mlandege FC katika mchezo wa nusu fainali utakaopigwa kesho Jumapili kwenye Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar.
Simba inatarajiwa kushuka dimbani huku ikiingia kwenye mchezo huo ikijua wazi haitakuwa kazi rahisi kutokana na ubora na historia ya wapinzani wao, Mlandege FC ambao ni moja ya timu zenye ushawishi mkubwa visiwani humo.
Akizungumza na wanahabari mapema leo, Kocha Steve Barker alisisitiza kuwa maandalizi ya timu yake yamekamilika na wachezaji wako tayari kupambana kuhakikisha wanapata matokeo chanya.
“Maandalizi ya mchezo huu yamekamilika, wachezaji wangu wako tayari kwenda kufanya kile kilicho bora,” alisema Barker.
Aidha, alikiri kuwa wanakutana na timu ngumu na yenye mafanikio Zanzibar, jambo linaloifanya mechi hiyo kuwa ya ushindani mkubwa zaidi.
“Tunafahamu haitakuwa mechi rahisi kwa sababu tunakwenda kucheza dhidi ya timu yenye mafanikio zaidi hapa Zanzibar,” aliongeza kocha huyo.
Hata hivyo, Barker alibainisha kuwa Simba haijapunguza malengo yake na ina imani kubwa ya kuvuka hatua hiyo muhimu.
“Lakini tuko tayari na tuna matumaini makubwa ya kupata ushindi na kusonga mbele hatua ya fainali,” alisisitiza.
Mlandege FC, ikiwa timu pekee kutoka visiwani Zanzibar iliyofanikiwa kufika hatua ya nusu fainali, inatarajiwa kupata sapoti kubwa ya mashabiki wake, jambo linaloweza kuongeza presha kwa Simba SC katika mchezo huo muhimu.
Endapo Simba itafanikiwa kushinda, itakutana na mshindi wa mchezo mwingine wa nusu fainali kati ya Azam FC na Yanga SC, ambao unatarajiwa kupigwa leo.



