Juzi klabu ya Simba ilishinda tuzo ya timu bora ya Mwaka 2025 tuzo zilizotolewa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kwa Taasisi na watu waliofanya vyema mwaka 2025.
Simba ilishinda tuzo hiyo baada ya kufika fainali ya kombe la Shirikisho mwaka 2025.
Hata hivyo tuzo hiyo ikamuibua Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe akihoji vigezo vilivyotumika kuipa Simba tuzo hiyo.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii, Kamwe alikumbusha namna mwaka 2023 Yanga ilivyotwaa tuzo hiyo kwa kuzingatia mafanikio kadhaa makubwa yaliyopatikana ndani na nje ya nchi.
Kwa mujibu wa Kamwe, mwaka huo Yanga ilipewa tuzo kutokana na:
- Kufika Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAFCC)
- Kutwaa Ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara
- Kushinda Kombe la Shirikisho la Azam
Kamwe ameonyesha kushangazwa na kile alichodai kuwa ni mabadiliko ya ghafla ya vigezo vya utoaji wa tuzo hizo.
“Mwaka 2023 sababu zilielezwa wazi kabisa mbele ya wadau wote. Leo tunaambiwa hatuna elimu na hatujui vigezo,” alihoji Kamwe.
Aidha, Kamwe amesema hali hiyo inaonyesha kuwa mafanikio ya ndani kama ubingwa wa ligi na makombe ya nyumbani hayapewi uzito mkubwa mbele ya mafanikio ya kufika hatua za mwisho katika michuano ya kimataifa.
Msimu uliopita Yanga ilitwaa mataji yote ya ndani yaani Ngao ya Jamii, Ligi Kuu, kombe la Mapinduzi, kombe la Muungano na kombe la CRDB lakini mataji hayo hayajatosha kwa Wananchi kushinda tuzo hiyo mbele ya watani zao Simba waliomaliza msimu mafanikio pekee yakiwa kucheza fainali ya CAFCC



