Kocha Mkuu wa Young Africans SC, Pedro Goncalves, amesema mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Pamba Jiji FC utakaopigwa kesho Jumatano, Aprili 8, katika Uwanja wa CCM Kirumba Stadium utakuwa mgumu kutokana na uimara wa wapinzani wao wanapocheza nyumbani.
Akizungumza na waandishi wa habari kuelekea mchezo huo, Goncalves alisema Pamba Jiji imejijengea rekodi ya kutopoteza mechi yoyote katika uwanja wake, jambo linaloifanya kuwa timu hatari hasa inapocheza mbele ya mashabiki wake.
“Tunakwenda kukutana na timu yenye ushindani mkubwa na imara wanapocheza nyumbani. Hawajapoteza mechi katika uwanja wao na timu nyingi kubwa zimekuja hapa bila kupata ushindi,” alisema.
Kocha huyo aliongeza kuwa wanatarajia mchezo wenye ushindani mkubwa na mazingira magumu, akieleza kuwa hali ya uwanja inaweza isiwe rafiki kwa soka la kuvutia, lakini hilo halitabadilisha malengo yao ya kutafuta ushindi.
“Tunapaswa kuwa imara, makini na kupambana ili kuhakikisha tunapata alama tatu,” alisisitiza.
Aidha, Goncalves alibainisha kuwa Pamba Jiji ni timu inayocheza kwa nguvu, kasi na kutumia vizuri faida ya mashabiki wao wa nyumbani, hali inayowalazimu Yanga kujiandaa kisaikolojia na kimkakati.
Katika hatua nyingine, kocha huyo alizungumzia ushindani wa ligi msimu huu, akisema licha ya timu yake kuwa juu ya msimamo, bado kuna safari ndefu mbele.
“Bado tuna michezo mingi na kila timu inapambana kufikia malengo yake, hivyo tunapaswa kuendelea kuwa makini na kufanya kazi kwa bidii,” alisema.
Aliongeza kuwa ana imani kubwa na wachezaji wake na wanahitaji kuonyesha nidhamu, umoja na ari ya kupambana ili kupata matokeo chanya katika mchezo huo.



