Inter watwaa taji la pili ndani ya wiki

Joel JJ By Joel JJ • 14th May 2026


Inter watwaa taji la pili ndani ya wiki

Inter Milan wameendelea kuthibitisha ubabe wao nchini Italia baada ya kutwaa taji la 10 la Coppa Italia kufuatia ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Lazio katika fainali iliyochezwa usiku wa Jumatano, Mei 13, 2026 kwenye dimba la Stadio Olimpico mjini Rome.

Mabingwa hao wa Serie A waliingia uwanjani wakiwa na morali kubwa baada ya tayari kutwaa Scudetto wiki iliyopita, na walionyesha ubora wao mapema kabisa kwenye mchezo huo.

Bao la kwanza lilitokana na kujifunga kwa Adam Marusic dakika ya 14 baada ya mpira wa kona wa Federico Dimarco kuleta taharuki ndani ya eneo la Lazio. Lautaro Martinez akaongeza bao la pili dakika ya 35 akimalizia pasi ya Marcus Thuram.

Ushindi huo umeifanya Inter kukamilisha “Domestic Double” yaani kutwaa Serie A pamoja na Coppa Italia ndani ya msimu mmoja. Hii ni mara ya kwanza kwa klabu ya Italia kufanya hivyo tangu Juventus msimu wa 2017–18.

Kocha mkuu Cristian Chivu ameandika historia kubwa katika msimu wake wa kwanza kuinoa Inter. Nahodha Lautaro Martinez amesema mafanikio hayo yametokana na nidhamu, umoja na hamu kubwa ya kushinda waliyoionyesha wachezaji wote msimu mzima.

Inter walitawala karibu kila eneo la mchezo huo huku kiungo Nicolò Barella na beki Denzel Dumfries wakitoa kiwango kikubwa. Lazio walijaribu kurejea kipindi cha pili kupitia Tijjani Noslin na Boulaye Dia lakini kipa Josep Martinez aliokoa hatari kadhaa muhimu.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.