Kocha Mkuu wa Azam FC, Florent Ibenge, ameibuka miongoni mwa makocha watano walioteuliwa na Shirikisho la Soka la Mali (FEMAFOOT) kuwania nafasi ya kocha mkuu wa timu ya taifa ya nchi hiyo, hatua inayoweza kubadilisha mustakabali wake katika klabu ya Azam FC.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Mali, jumla ya maombi 28 yaliwasilishwa kwa ajili ya nafasi hiyo, kabla ya kamati ya ufundi kufanya mchujo uliobaki na majina matano ya mwisho, likiwemo la Ibenge, ambaye kwa sasa anaifundisha Azam FC ya Tanzania.
Makocha wengine waliobaki kwenye kinyang'anyiro hicho ni pamoja na Badou Zaki, pamoja na makocha kutoka Ureno na Mali, katika mchakato unaoendelea kuelekea uteuzi wa mwisho wa kocha huyo mpya wa “Eagles” wa Mali.
MUSTAKABALI WA AZAM FC WAKO HATARINI
Taarifa hizi zimezidi kuongeza mjadala ndani ya Azam FC, ambapo Ibenge bado ana mkataba unaoelekea ukingoni mwishoni mwa msimu huu, huku mazungumzo ya kuongeza mkataba mpya yakielezwa kusimama kwa muda.
Endapo atateuliwa kuinoa Mali, kuna uwezekano mkubwa wa klabu hiyo ya Jiji la Dar es Salaam kulazimika kuanza mchakato wa kutafuta kocha mpya kuelekea msimu ujao.
REKODI YAKE BARANI AFRIKA
Ibenge anasifika kwa mafanikio makubwa katika soka la Afrika, akiwa amewahi:
- Kuinoa timu ya taifa ya DR Congo
- Kufika hatua kubwa za michuano ya AFCON
- Kushinda Kombe la CAF Confederation Cup akiwa na RS Berkane
- Kufundisha vilabu mbalimbali ikiwemo Al Hilal na AS Vita Club
Uzoefu wake huo ndio unaomfanya kuwa miongoni mwa majina yanayopewa nafasi kubwa katika mchakato wa Mali.



