Mbio za kuwania tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwezi Mei 2026 katika Ligi Kuu ya NBC zimezidi kushika kasi, huku mastaa watatu wakionyesha ubora wa hali ya juu na kuibua mjadala mkali miongoni mwa mashabiki na wachambuzi wa soka nchini.
Wachezaji hao ni Feisal Salum wa Azam FC, Allan Okello wa Yanga SC na Clatous Chama wa Simba SC, ambao kila mmoja ameweka takwimu zenye ushindani mkubwa ndani ya mwezi mmoja wa mashindano.
Kwa mujibu wa takwimu za mwezi Mei pekee, Okello ameonekana kuwa na mwenendo mzuri zaidi wa mabao, akifunga mabao 9 na kutoa pasi za mabao 1, huku akihusika kwenye jumla ya mabao 10 na kuchukua tuzo ya Mchezaji Bora wa Mechi mara nne.
Feisal Salum “Fei Toto” wa Azam FC naye ameendelea kuonesha kiwango cha juu zaidi katika msimu mzima, akiwa kinara wa mabao kwenye ligi kwa jumla ya mabao 14 na asisti 8. Katika mwezi Mei, ameweka mabao 7 na asisti 1, akihusika kwenye jumla ya mabao 8 na kuchukua tuzo ya Mchezaji Bora wa Mechi mara tatu.
Kwa upande wake, Clatous Chama wa Simba SC ameendelea kuthibitisha ubora wake kama kiungo mshambuliaji mwenye ubunifu mkubwa, akiwa na mabao 8 na asisti 6 kwa msimu mzima. Mwezi Mei ameweka mabao 5 na asisti 4, huku akiongoza kwa idadi ya tuzo za Mchezaji Bora wa Mechi mara tano.
Mchambuzi wa soka ameeleza kuwa ushindani wa tuzo ya mwezi bado uko wazi, kutokana na kila mchezaji kuwa na sifa tofauti zinazoangaliwa Okello akiwa na nguvu ya moja kwa moja kwenye mabao, Feisal akiwa kinara wa msimu mzima, na Chama akiwa na ushawishi mkubwa wa mchezo pamoja na tuzo nyingi za MOTM.
Ni wazi, uamuzi wa mwisho wa mchezaji bora wa mwezi Mei 2026 unatarajiwa kuwa mgumu zaidi kutokana na ubora wa karibu kati ya mastaa hao watatu, huku mashabiki wakisubiri kwa hamu matokeo rasmi.



