Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF) limethibitisha rasmi kuwa droo ya michuano ya kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 itafanyika tarehe 19 Mei 2026, hatua itakayoweka ramani ya safari ya mataifa 48 yanayowania nafasi ya kushiriki fainali za AFCON PAMOJA 2027.
Kwa mujibu wa CAF, droo hiyo itahusisha jumla ya timu 48, ikiwa ni pamoja na wenyeji wenza wa mashindano hayo, Kenyha, Tanzania na Uganda ambao tayari wamefuzu moja kwa moja kama wenyeji wa fainali hizo zitakazofanyika kwa pamoja katika nchi hizo tatu za Afrika Mashariki.
Mfumo wa makundi
Katika droo hiyo, timu 48 zitapangwa kwenye makundi 12, kila kundi likiwa na timu nne. Kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa, timu mbili za juu katika kila kundi zitafuzu moja kwa moja kwenda fainali za AFCON 2027.
Mfumo huo unatarajiwa kuongeza ushindani mkubwa, ambapo kila mchezo wa kufuzu utakuwa na umuhimu wa moja kwa moja katika kuhakikisha timu inasonga mbele au kuondolewa katika mbio za kufuzu.
Ratiba ya mechi za kufuzu
CAF pia imetangaza vipindi vitakavyotumika kwa mechi za hatua ya makundi kama ifuatavyo:
- Septemba hadi Oktoba 2026
- Novemba 2026
- Machi 2027
Vipindi hivyo vitatumika kukamilisha ratiba ya timu zitakazofuzu na kujiunga na mataifa wenyeji katika fainali za 2027.
AFCON PAMOJA 2027
Michuano ya AFCON 2027, maarufu kama AFCON PAMOJA 2027, itakuwa ya kihistoria kwa kuwa itafanyika kwa mara ya kwanza katika mataifa matatu kwa pamoja ya Afrika Mashariki. Mashindano hayo yanatarajiwa kuongeza hadhi ya soka katika ukanda huo na kuvutia mashabiki kutoka pembe zote za dunia.



