Droo ya kupanga makundi ya michuano ya kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 inatarajiwa kufanyika Jumanne, Mei 19, 2026, katika hafla inayosubiriwa kwa hamu kubwa na mataifa mbalimbali barani Afrika.
Kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), droo hiyo itaamua mfumo wa makundi yatakayoanza safari ya timu 48 kuelekea fainali za AFCON 2027 zitakazofanyika nchini Kenya, Uganda na Tanzania.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa sherehe hiyo itafanyika Cairo, Misri saa 9 Alasiri, huku maandalizi yakiwa yamekamilika kwa ajili ya kuhakikisha droo inafanyika kwa uwazi na viwango vya juu vya kiutawala kama ilivyo kawaida ya CAF.
Kwa mujibu wa CAF, michuano ya kufuzu itahusisha jumla ya timu 48, ikiwa ni pamoja na mataifa matatu wa wenyeji ambao tayari wamepata nafasi ya moja kwa moja katika fainali. Mfumo huo utatoa nafasi kwa mataifa 24 kufuzu kwenye mashindano ya mwisho.
AFCON 2027 yenyewe itakuwa ya kihistoria kwa Afrika Mashariki, ikiwa ni mara ya kwanza kwa mataifa matatu Kenya, Uganda na Tanzania kushirikiana kuiandaa michuano hiyo mikubwa ya soka barani Afrika.
Michuano hiyo inatarajiwa kufanyika kuanzia Juni 19 hadi Julai 17, 2027, ambapo maandalizi ya viwanja na miundombinu yameendelea katika nchi zote tatu wenyeji ili kuhakikisha mashindano yanakuwa ya kisasa na yenye viwango vya kimataifa.



