Mashabiki waliojazana katika Uwanja wa Airtel Mtipa hawatausahau mchezo huu kwa haraka. Ilikuwa ni mechi yenye kila aina ya hisia, presha, furaha na majonzi baada ya Dodoma Jiji FC kuibuka na ushindi wa kihistoria wa mabao 3-2 dhidi ya Young Africans SC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa leo Mei 13, 2026.
Matokeo hayo yameandika historia mpya kwa Yanga, kwani ni mara ya kwanza kwa mabingwa hao watetezi kupoteza mchezo wa ligi msimu huu baada ya kuwa katika mwendo mzuri wa kutopoteza kwa mechi 42 mfululizo.
Mchezo ulianza kwa kasi huku Yanga wakionyesha dhamira ya kuendelea kulinda rekodi yao ya kutopoteza. Kiungo mshambuliaji mahiri Allan Okello alikuwa mwiba kwa safu ya ulinzi ya Dodoma Jiji na ndiye aliyeipa Yanga bao la kwanza kwa shuti kali ndani ya 18.
Hata hivyo, wenyeji hawakukata tamaa. Shinikizo lao lilizaa matunda baada ya nahodha wa Yanga Bakari Mwamnyeto kujifunga bao lililoirudisha Dodoma Jiji mchezoni na kufanya matokeo kuwa 1-1.
Dakika chache baadaye, Allan Okello alirejea tena kuifungia Yanga bao la pili na kuwapa matumaini mashabiki wa Wananchi. Mpaka dakika ya 87, Yanga walikuwa mbele kwa mabao 2-1 na wengi waliamini pointi tatu zilikuwa mikononi mwao, lakini kandanda huwa halitabiriki.
Dakika Tano za Maafa kwa Wananchi
Dakika za mwisho zilikuwa za simanzi kwa Yanga na furaha kubwa kwa Dodoma Jiji. Katika kipindi ambacho Yanga walionekana kucheza kwa tahadhari wakisubiri filimbi ya mwisho, Dodoma Jiji waliinua morali na kushambulia kwa nguvu.
Mshambuliaji Kibuta aliisawazishia Dodoma Jiji katika dakika za lala salama, bao lililowapa nguvu wenyeji kuamini wanaweza kufanya makubwa zaidi.
Yanga walipojaribu kusaka bao la ushindi kwa mashambulizi ya haraka, walijikuta wakinaswa kwenye shambulizi la kushtukiza. Dakika ya 95, Waziri Junior Shentembo akafunga bao la tatu lililowazamisha Wananchi na kuipa Dodoma Jiji ushindi wa 3-2.
Bao hilo lilizua shangwe kubwa kwa mashabiki wa Dodoma Jiji huku benchi la Yanga likibaki katika mshangao mkubwa.
Matokeo haya yanaifanya Dodoma Jiji kuandika ushindi muhimu dhidi ya Yanga ambao kwa miaka ya karibuni wamekuwa na ubabe mkubwa kwenye rekodi za timu hizo mbili. Kabla ya mchezo huu, Yanga walikuwa wameishinda Dodoma Jiji mara nyingi mfululizo, ikiwemo ushindi wa mabao 3-1 walioupata Januari mwaka huu katika Uwanja wa KMC Complex.
Kwa upande wa Yanga, mchezo huu unaacha maswali mengi kuhusu umakini wa safu yao ya ulinzi eneo lao la ushambuliaji ambalo lilipoteza nafasi nyingi
Matokeo hayo yanaiongezea Yanga presha kwenye mbio za ubingwa kwani kama Simba itashinda mchezo wake dhidi ya Mashujaa Fc, tofauti ya alama baina ya timu hizo itakubwa mbili tu.



