Klabu ya Chelsea imefanikiwa kutinga fainali ya Kombe la FA baada ya ushindi mwembamba wa mabao 1-0 dhidi ya Leeds United katika nusu fainali iliyochezwa dimbani Wembley.
Bao pekee la mchezo huo lilifungwa na kiungo nyota Enzo Fernándezdakika ya 23, akimalizia vizuri mpira wa krosi uliopigwa ndani ya boksi.
Licha ya kuonyesha ubora mkubwa kipindi cha kwanza, Chelsea walilazimika kujilinda kwa nguvu katika kipindi cha pili, huku kipa wao Robert Sánchez akiokoa michomo kadhaa hatari kutoka kwa wapinzani wao.
Ushindi huo unakuja katika kipindi kigumu kwa Chelsea kufuatia kuondoka kwa kocha wao wa zamani, huku kocha wa muda Calum McFarlane akiiongoza timu hiyo kufika hatua hiyo muhimu.
Upande mwingine, mabingwa wa soka la England Manchester City jana walifanikiwa kufika fainali baada ya kuifunga Southampton kwa mabao 2-1.
City walitoka nyuma na kufanya “comeback” ya kusisimua katika dakika za mwisho za mchezo huo, wakionyesha ubora wao na uzoefu mkubwa kwenye michuano mikubwa.
Hii ni mara ya nne mfululizo kwa Manchester City kufika fainali ya FA Cup, jambo linaloonyesha ubabe wao katika soka la England kwa miaka ya hivi karibuni.
Mchezo wa fainali kati ya Chelsea dhidi ya Manchester City utapigwa katika dimba la Wembley tarehe 16 Mei 2026.
Hii itakuwa mara ya kwanza kwa timu hizi mbili kukutana katika fainali ya FA Cup, na kufanya mchezo huo kutarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.
Chelsea wanatafuta taji lao la tisa la FA Cup, huku Manchester City wakisaka kuongeza rekodi yao na kuendelea na mafanikio yao ya hivi karibuni.



