Klabu ya Chelsea imeanza rasmi mchakato wa kutafuta kocha mpya kuelekea msimu ujao, huku majina kadhaa makubwa yakitajwa kuwania nafasi hiyo muhimu ndani ya Stamford Bridge, kama ilivyoripotiwa na Fabrizio Romano.
Hatua hiyo inakuja wakati klabu hiyo ikipitia kipindi kigumu cha matokeo na mabadiliko ya mara kwa mara ya benchi la ufundi, hali inayolazimisha uongozi kutafuta suluhisho la kudumu.
Miongoni mwa makocha wanaotajwa kupewa nafasi kubwa ni Andoni Iraola, ambaye ameonyesha mafanikio makubwa akiwa na AFC Bournemouth. Iraola anasifiwa kwa mtindo wake wa kisasa wa soka unaochanganya nguvu, kasi na mbinu, pamoja na uzoefu wake ndani ya Premier League.
Pia anatajwa Filipe Luís, ambaye kwa sasa anaongoza CR Flamengo kwa mafanikio. Akiwa mchezaji wa zamani wa Chelsea, anaifahamu vyema klabu hiyo, ingawa uzoefu wake kama kocha barani Ulaya bado ni mdogo.
Chaguo jingine ni Frank Lampard, legenda wa klabu hiyo ambaye tayari aliwahi kuinoa timu hiyo hapo awali. Lampard anaungwa mkono na sehemu ya mashabiki, lakini kumbukumbu ya matokeo yake ya mwisho akiwa kocha bado inaibua maswali.
Aidha, jina la Cesc Fàbregas pia linatajwa, kufuatia kazi yake nzuri akiwa na Como 1907 nchini Italia. Hata hivyo, uzoefu wake mdogo katika miradi mikubwa unatajwa kuwa changamoto inayoweza kuathiri nafasi yake.
Majina mengine yanayotajwa kuhusishwa kurithi mikoba ya Rosenior ni kama, Marco Silver (Fulham), Xabi alonso na Luis Enrique (PSG).
Chelsea wanaripotiwa kupanga kufanya mabadiliko makubwa majira ya joto, ikiwa ni pamoja na kusajili wachezaji wenye uzoefu zaidi ili kuleta uwiano ndani ya kikosi, pamoja na kumpa kocha mpya nafasi ya kushiriki moja kwa moja katika maamuzi ya usajili.
Tangu mwaka 2021, klabu hiyo imebadilisha makocha mara kadhaa, hali inayochochea hitaji la kupata suluhisho la muda mrefu litakalorejesha utulivu na ushindani ndani ya timu.
Kwa sasa, macho yote yanaelekezwa Stamford Bridge huku wadau wakisubiri kuona nani atapewa jukumu la kuiongoza Chelsea katika sura mpya ya klabu hiyo.



