Klabu ya Chelsea inaripotiwa kukumbwa na hali ngumu ya ndani, huku mustakabali wa kocha Liam Rosenior ukiwa mashakani kufuatia mwenendo mbaya wa timu hiyo katika siku za hivi karibuni.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka TEAMtalk, kuna hali ya kutoridhika ndani ya kikosi, hasa kutokana na ukosefu mkubwa wa mabao kutoka kwa safu ya ushambuliaji. Wachezaji kadhaa waliosajiliwa kwa gharama kubwa wameshindwa kuonesha makali yao, hali inayozua maswali kuhusu mfumo wa timu pamoja na maamuzi ya benchi la ufundi.
Inaelezwa kuwa imani ya viongozi wa klabu kwa Rosenior imeanza kuyumba licha ya hapo awali kuonyesha matumaini nae hata kama klabu ikishindwa kushiriki Champions League msimu ujao, huku baadhi ya wachezaji wakuu wakionyesha kutoridhishwa na mwelekeo wa timu. Vyanzo vinaeleza kuwa kuna hisia miongoni mwa kikosi kwamba timu inahitaji kocha mwenye uzoefu zaidi ili kurejesha ushindani.
Aidha, uamuzi wa awali wa kumtimua aliyekuwa kocha Enzo Maresca umeanza kutajwa kama moja ya sababu zilizochangia hali ya sasa, huku baadhi ya viongozi ndani ya klabu wakidaiwa kukiri kuwa hatua hiyo inaweza kuwa ilichukuliwa kwa haraka.
Kutokana na hali hiyo, kuna uwezekano wa mabadiliko ya kiufundi kufanyika katika kipindi kijacho, iwapo matokeo hayataboreka. Majina mbalimbali ya makocha wenye uzoefu yameanza kuhusishwa na nafasi hiyo ikiwa jina la kocha wa Atletico Madrid Diego Simione, ingawa bado hakuna maamuzi rasmi yaliyotangazwa.
Kwa sasa, presha inaendelea kuongezeka ndani ya Stamford Bridge, huku mashabiki wakisubiri hatua madhubuti zitakazorejesha timu hiyo katika mstari wa ushindani.



