Chama mbioni kuongeza mkataba mpya Simba

Joel JJ By Joel JJ β€’ 21st May 2026


Chama mbioni kuongeza mkataba mpya Simba

Kiungo mshambuliaji Clatous Chama anatarajiwa kuendelea kuitumikia Simba SC baada ya kuingia kwenye hatua za mwisho za mazungumzo ya kuongeza mkataba mpya ndani ya kikosi hicho cha Wekundu wa Msimbazi, imefahamika.

Chama, ambaye alirejea Simba akitokea Singida Big Stars SC, alisaini awali mkataba wa mwaka mmoja, lakini sasa taarifa zinaeleza kuwa mazungumzo ya kuongeza kandarasi ya ziada ya mwaka mmoja yamekamilika kwa mafanikio.

Kwa mujibu wa vyanzo kutoka ndani ya uongozi wa Simba, mkataba mpya wa kiungo huyo sasa unatarajiwa kumfanya abaki klabuni hapo hadi mwaka 2028, hatua inayoonekana kuwa sehemu ya mkakati wa klabu kuimarisha kikosi chake cha ushindani.

Uongozi wa Simba umechukua hatua ya mapema kuhakikisha nyota huyo anasaini mkataba mpya kabla ya msimu wa mashindano kufikia tamati, ili kuondoa uwezekano wa vilabu vingine kuingia kwenye vita ya kumsajili.

Tangu aliporejea Msimbazi kupitia dirisha dogo, Chama ameendelea kuwa mchezaji muhimu katika mfumo wa timu, akichangia mabao nane katika mashindano yote na kuonyesha kiwango kinachovutia mashabiki na wadau wa soka nchini.

Mbali na mchango wake wa mabao, kiungo huyo kutoka Zambia pia ameweka rekodi ya kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa mchezo katika mechi nne mfululizo, hali inayoonyesha ubora wake na umuhimu wake ndani ya kikosi cha Simba.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.