Klabu ya Bayern Munich imeendelea kuonyesha ubabe wake katika Bundesliga baada ya kuibuka na ushindi wa kusisimua wa mabao 4-3 dhidi ya Mainz 05 katika mchezo uliochezwa Jumamosi, Aprili 25, 2026.
Katika mchezo huo wa kusisimua uliopigwa kwenye dimba la MEWA Arena, Bayern walijikuta wakicheza chini ya kiwango kipindi cha kwanza baada ya kuruhusu mabao matatu kutoka kwa Mainz, yaliyofungwa na Dominik Kohr, Paul Nebel na Sheraldo Becker.
Hata hivyo, mabingwa hao tayari wa Bundesliga walirudi kwa nguvu kipindi cha pili na kuonyesha kwa nini wanaitwa mabingwa. Nicolas Jackson alianza kurejesha matumaini kwa kufunga bao la kwanza dakika ya 53 kabla ya Michael Olise kupunguza pengo zaidi dakika ya 73.
Shinikizo liliendelea kuongezeka kwa Mainz baada ya Jamal Musiala kusawazisha dakika ya 80, kabla ya mshambuliaji hatari Harry Kane kufunga bao la ushindi dakika ya 83 na kukamilisha comeback ya ajabu.
Ushindi huo unaifanya Bayern kuendeleza rekodi yao nzuri ya ushindi mfululizo, ikiwa ni moja ya dalili za uimara mkubwa waliouonyesha msimu huu.
Bayern tayari walikuwa wametangazwa mabingwa wa Bundesliga kabla ya mchezo huo, baada ya ushindi wao dhidi ya Stuttgart uliowahakikishia taji la msimu wa 2025/26.



