Klabu ya Bayern Munich, leo Jumatano inashuka dimbani kwenye mtanange mzito wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Paris Saint-Germain (PSG), mchezo unaotajwa kuwa wa “kufa au kupona” kwa miamba hao wa Ujerumani.
Mchezo huo wa mkondo wa pili unachezwa katika dimba la Allianz Arena, huku Bayern wakiwa na kazi kubwa ya kupindua matokeo baada ya kufungwa 5-4 katika mchezo wa kwanza uliopigwa jijini Paris.
Kutokana na matokeo hayo, Bayern Munich wanahitaji ushindi wa angalau mabao mawili ili kufuzu moja kwa moja kwenda fainali, au ushindi wa bao moja kisha kulazimisha mchezo kuingia hatua ya mikwaju ya penalti.
Katika mchezo wa kwanza, mashabiki walishuhudia tamasha la soka lenye mabao mengi, ambapo PSG walionyesha ubora wao wa kushambulia huku Bayern nao wakionyesha uwezo mkubwa wa kurejea mchezoni licha ya kuwa nyuma kwa mabao kadhaa.
Kocha wa PSG, Luis Enrique, anaingia kwenye mchezo huu akiwa na matumaini ya kutinga fainali kwa mara ya pili mfululizo, huku akitambua ubora wa Bayern Munich ambao ameutaja kuwa miongoni mwa timu ngumu zaidi kukutana nazo.
Kwa upande wa Bayern, matumaini yao makubwa yako kwa safu yao kali ya ushambuliaji pamoja na faida ya kucheza nyumbani, ambapo wamekuwa na rekodi nzuri ya kufunga mabao mengi katika michuano ya Ulaya msimu huu.
Mshindi wa pambano hili atakutana na Arsenal kwenye fainali ya michuano hiyo itakayopigwa jijini Budapest baadaye mwezi huu, jambo linaloongeza uzito na presha ya mchezo wa leo.



