Kesho Jumapili, Aprili 19, macho ya mashabiki wa soka nchini yataelekezwa katika Uwanja wa Majaliwa ambapo Simba SC watashuka dimbani kuikabili Namungo FC katika mchezo wa Ligi Kuu wenye ushindani mkubwa.
Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker, ameweka wazi kuwa kikosi chake kipo tayari kikamilifu kwa ajili ya pambano hilo. Akizungumza na wanahabari kuelekea mchezo huo, Barker alisisitiza kuwa licha ya kutambua ugumu wa mpinzani wao, maandalizi yamekamilika kwa kiwango cha juu.
“Tunajua haitakuwa mechi rahisi kwa sababu Namungo ni timu imara, lakini sisi tumejiandaa vizuri kuhakikisha tunapata alama tatu,” alisema Barker.
Kocha huyo aliongeza kuwa falsafa ya Simba haitabadilika katika mchezo huo. Amesema timu yake itaendelea kucheza soka la kuvutia, lenye ushindani na matokeo chanya kwa mashabiki wao.

Kwa upande wa Namungo, Kocha Mkuu Juma Mgunda naye ameonesha kujiamini kuelekea mchezo huo. Amesema maandalizi ya timu yake yamekamilika na sasa jukumu limebaki kwa wachezaji kutekeleza maelekezo waliyopewa.
“Maandalizi mazuri yamekamilika. Sasa ni kwa wachezaji kuonyesha walichojifunza uwanjani. Tuko tayari kushindana na Simba,” alisema Mgunda.
Mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa huku kila timu ikihitaji ushindi ili kuimarisha nafasi yake kwenye msimamo wa ligi.



