Barcelona yanusa ubingwa La Liga

Joel JJ By Joel JJ • 23rd April 2026


Barcelona yanusa ubingwa La Liga

Klabu ya FC Barcelona imepiga hatua kubwa kuelekea kutwaa ubingwa wa La Liga baada ya kuibuka na ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Celta Vigo katika mchezo uliopigwa Jumatano usiku, April 22, 2026.

Bao pekee la ushindi lilifungwa na kinda nyota Lamine Yamal dakika ya 38 kwa njia ya penalti, baada ya yeye mwenyewe kuchezewa madhambi ndani ya eneo la hatari.

Ushindi huo umeifanya Barcelona kufikisha pointi 82 kileleni mwa msimamo, ikiwaacha wapinzani wao wakubwa Real Madrid kwa tofauti ya pointi tisa huku zikiwa zimesalia mechi sita tu kumalizika kwa msimu. 

Matokeo hayo yanaifanya Barcelona kuwa katika nafasi nzuri sana ya kutwaa ubingwa wa La Liga msimu huu, wakihitaji matokeo machache tu kuthibitisha taji hilo.

Hata hivyo, ushindi huo umeambatana na pigo kubwa baada ya Lamine Yamal kupata majeraha mara baada ya kufunga penalti hiyo. Nyota huyo alionekana kushika misuli ya paja (hamstring) na kulazimika kutolewa uwanjani muda mfupi baada ya kufunga bao hilo. 

Tukio hilo limeibua wasiwasi mkubwa kwa benchi la ufundi la Barcelona likiongozwa na kocha Hansi Flick, hasa ikizingatiwa umuhimu wa Yamal katika kikosi hicho na mechi ngumu zilizobaki ikiwemo El Clasico inayokuja. 

Licha ya Barcelona kutawala sehemu kubwa ya mchezo, Celta Vigo walitoa upinzani mkali na kutengeneza nafasi kadhaa za kufunga, lakini walishindwa kuzitumia ipasavyo. VAR pia iliwanyima Barcelona bao la pili lililofungwa na Ferran Torres kutokana na kuotea.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.