Ni kama kiungo mshambuliaji wa Simba SC Mohamed Bajaber, amepewa nafasi ya kujitetea ili kurejea rasmi kikosini baada ya kukumbwa na mfululizo wa majeraha yaliyomuweka nje kwa muda mrefu.
Bajaber alirejea uwanjani jana baada ya kukosekana kwa muda mrefu, alipokuwa sehemu ya kikosi cha Simba kilichocheza robo fainali ya Kombe la Muungano dhidi ya Mafunzo FC. Katika mchezo huo, Simba ilitinga hatua ya nusu fainali baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0.
Tangu ajiunge na Simba akitokea Polisi FC katika dirisha la usajili la Julai mwaka jana, mchezaji huyo hajapata nafasi ya kuonyesha kiwango chake kutokana na kusumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara.
Majeraha hayo yamekuwa kikwazo kikubwa kwake pamoja na mashabiki wa Simba waliokuwa na matarajio ya kushuhudia uwezo wake uwanjani.
Kutokana na hali hiyo, uongozi wa Simba ulilazimika kumuondoa kwenye mfumo wa usajili katika dirisha dogo ili kutoa nafasi kwa mchezaji mwingine wa kigeni, huku ukimpa muda wa kuimarika kiafya.
Hata hivyo, Bajaber aliendelea kufanya mazoezi na kikosi hicho, jambo linaloashiria kuwa bado yupo kwenye mipango ya timu hiyo.
Kurejea kwake kupitia michuano ya Kombe la Muungano kunaonekana kuwa ni mwanzo wa juhudi zake za kujithibitisha upya ili kurejeshwa rasmi kikosini.
Bajaber bado ana mkataba wa muda mrefu na Simba, huenda Wekundu hao wa Msimbazi wakamrejesha kikosini kwenye dirisha lijalo la usajili kama watajiridhisha amepona sawa sawa na anaweza kutumika.
Lakini kama mambo yatakuwa tofauti huenda kwenye wakati mgumu zaidi kwani huenda mabosi wa Simba wasiwe na muda mrefu zaidi wa kumsubiri hasa ikizingatiwa ni mchezaji wa kigeni.



