Azam FC imeibuka na ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya JKT Tanzania katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC uliopigwa Ijumaa, Aprili 17, 2026, kwenye Uwanja wa Azam Complex.
Azam FC ilipata ushindi wake katika kipindi cha pili, Japhet Kitambala akifungua ukurasa wa mabao kabla ya Iddy Nado kufunga mabao mawili yaliyokamilisha ushindi huo mnono.
Kipindi cha kwanza cha mchezo kilimalizika bila kufungana (0-0), huku timu zote zikionyesha ushindani mkali na tahadhari kubwa katika safu za ulinzi.
Baada ya mapumziko, Azam FC walirudi uwanjani kwa kasi na kushambulia kwa nguvu, hatua iliyowawezesha kupata bao la uongozi kupitia Kitambala dakika za mwanzo za kipindi cha pili.
Feisal Salum 'Fei Toto' alikuwa tishio kwa JKT Tanzania akitoa pasi za mabao mawili na sasa akiongoza orodha ya vinara wa asisti akifikisha saba.
JKT Tanzania walijaribu kufanya mashambulizi ya kusawazisha lakini walikosa umakini katika umaliziaji pamoja na kukutana na ulinzi imara wa Azam FC.
Ushindi huo unaifanya Azam FC izidi kujiimarisha kwenye nafasi ya tatu ikifikisha alama 37, alama mbili nyuma ya Simba inayoshika nafasi ya pili.
Kipigo kwa JKT Tanzania kimewashusha hadi nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi nyuma ya Singida BS wakiwa na alama sawa 29 tofauti ikiwa uwiano wa mabao



