Mikel Arteta ameendelea kuonyesha namna anavyotumia mbinu za kipekee kuwajenga kisaikolojia wachezaji wa Arsenal, baada ya kuweka mfano wa kombe la Premier League katika uwanja wa mazoezi wa timu. Lakini kombe hilo lina tofauti moja kubwa, limeunganishwa na mfumo wa taa na linaweza kuwaka tu pale Arsenal watakapothibitishwa kuwa mabingwa.
Kwa siku zote za msimu, kombe hilo limekuwa pale mazoezini likiwa kimya, bila mwanga, kama ukumbusho wa kila siku kwa kikosi kwamba kazi bado haijakamilika. Wachezaji wamekuwa wakilipita kila wanapoingia mazoezini, wakilitazama kama lengo la mwisho ambalo bado hawajalifikia. Arteta ameonekana kutaka ndoto hiyo iwe mbele ya macho yao kila siku, si kwenye maneno pekee.
Hatua hiyo inakuja wakati Arsenal wako kileleni mwa msimamo wa ligi, wakiwa wamebakiza mechi mbili pekee kumaliza msimu ambazo ni dhidi ya Burnley wakiwa home na Crystal Palace wakiwa ugenini. Mbio za ubingwa bado ziko wazi huku Manchester City wakiendelea kufuatilia kwa karibu, lakini Arsenal wana nafasi nzuri ya kumaliza kazi na kubeba kombe hilo kwa mara ya kwanza mbele ya kikosi chao.
Mbinu za Arteta zimekuwa zikizungumziwa sana msimu huu. Mbali na kombe hilo, amewahi kutumia mbinu za kisaikolojia kama picha za mbwa wawindaji na hata njia nyingine za kuhamasisha kikosi kabla ya mechi kubwa. Ni njia zinazoonyesha jinsi anavyotaka wachezaji waishi ndoto hiyo kila siku, hadi ije kuwa ukweli.
Kwa wachezaji kama Bukayo Saka, Gabriel Martinelli na Kai Havertz, kombe hilo si mapambo tu. Limekuwa ishara ya kile wanachopigania. Kila mazoezi, kila jasho, kila mechi β macho yao yanarudi kwenye kitu kilekile: taji (Ubingwa)
Sasa Arsenal wako hatua mbili tu kutoka kutimiza ndoto hiyo. Kama watamaliza kazi yao, kombe hilo litawaka kwa mara ya kwanza β na kitendo hicho kinaweza kuwa picha moja itakayosimulia safari nzima ya msimu huu. Wakati mwingine, ishara ndogo hujenga historia kubwa



