Klabu ya Arsenal imefanikiwa kurejea kileleni mwa msimamo wa Premier League baada ya kuibuka na ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Newcastle United katika mchezo uliochezwa Jumamosi, Aprili 25, 2026, kwenye dimba la Emirates.
Bao pekee la mchezo lilifungwa mapema katika dakika ya tisa na kiungo mshambuliaji Eberechi Eze, aliyepiga shuti kali nje ya eneo la hatari kufuatia mpira wa kona uliopangwa kwa ustadi, na kumshinda kipa Nick Pope.
Arsenal walianza mchezo huo kwa kasi wakionyesha dhamira ya kupata ushindi mapema, huku wakidhibiti sehemu kubwa ya kipindi cha kwanza. Licha ya Newcastle United kujaribu kusawazisha katika dakika za baadaye, safu ya ulinzi ya wenyeji ilisimama imara kuzuia mashambulizi yote.
Katika kipindi cha pili, Newcastle waliongeza presha wakitafuta bao la kusawazisha, lakini walishindwa kutumia nafasi walizopata, huku Arsenal wakicheza kwa nidhamu na kulinda bao lao hadi mwisho wa mchezo.
Ushindi huo unaifanya Arsenal kufikisha jumla ya pointi 73 na kurejea kileleni mwa msimamo wa ligi, hatua inayowapa nguvu mpya katika mbio za ubingwa huku msimu ukielekea ukingoni.
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta, alisifu juhudi za wachezaji wake kwa kuonyesha nidhamu na umakini mkubwa, akieleza kuwa ushindi huo ni muhimu katika hatua ya mwisho ya msimu.
Kwa upande wao, Newcastle United walionyesha ushindani mkali lakini walikosa umakini katika umaliziaji wa nafasi, jambo lililowagharimu kupata matokeo chanya ugenini.
Wapinzani wakuu wa Arsenal katika mbio za ubingwa Manchester City wanaweza kurejea kileleni kama watashinda mechi yao ya kiporo.
Jana Man City walikuwa uwani kucheza mechi ya nusu fainali kombe la FA wakiibuka na ushindi wa mabao 2-1



