Alvarez azidi kuiweka gizani Atletico Madrid

Joel JJ By Joel JJ • 25th May 2026


Alvarez azidi kuiweka gizani Atletico Madrid

Mshambuliaji wa kimataifa wa Argentina, Julián Álvarez, hana mpango wa kuongeza mkataba mpya na Atlético Madrid kwa sasa licha ya taarifa zinazoendelea kuhusisha mazungumzo ya kuboresha mkataba wake ndani ya klabu hiyo.

Hatua hiyo imeongeza uvumi kuhusu mustakabali wa nyota huyo wa zamani wa Manchester City, ambaye tayari anawindwa na vigogo mbalimbali wa Ulaya akiwemo FC Barcelona, Paris Saint-Germain pamoja na baadhi ya klabu za Premier League.

Kocha wa Atlético Madrid, Diego Simeone, alizungumza wazi kuhusu hali ya mshambuliaji huyo baada ya mchezo wa mwisho wa La Liga dhidi ya Villarreal, akionyesha kuwa maamuzi ya mchezaji huyo yako mikononi mwake mwenyewe.

“Future ya Álvarez? Hilo si swali langu, ni swali lake. Ana umri wa kutosha kujua anachotaka kufanya na naamini tayari ameshafanya maamuzi yake,” alisema Simeone.

BARCELONA, PSG NA EPL ZAMUWANIA

Taarifa kutoka Hispania na Ufaransa zinaeleza kuwa Barcelona wanaendelea kumtazama Álvarez kama mbadala wa mshambuliaji mkongwe Robert Lewandowski, huku PSG nao wakitajwa kuwa tayari kuingia kwenye vita ya usajili wake.

Aidha, klabu za England zikiwemo Arsenal F.C. zimeonyesha nia ya kumrejesha mshambuliaji huyo Premier League baada ya mafanikio aliyoyapata akiwa Manchester City chini ya Pep Guardiola.

NGUZO MUHIMU ATLETICO

Tangu ajiunge na Atlético Madrid mwaka 2024 akitokea Manchester City kwa ada iliyovunja rekodi ya klabu hiyo, Álvarez amekuwa mmoja wa nyota muhimu ndani ya kikosi cha Simeone.

Msimu huu ameendelea kuonyesha kiwango bora katika La Liga na michuano ya Ulaya, jambo linalofanya Atlético kutokuwa tayari kumuachia kirahisi licha ya presha kutoka kwa vilabu vikubwa Ulaya.

Hata hivyo, kusuasua kwa mazungumzo ya kuongeza mkataba mpya kunaendelea kuongeza uwezekano wa mshambuliaji huyo kuondoka ndani ya dirisha lijalo la usajili.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.