Klabu ya Al Ahly SC imewasilisha ombi rasmi kwa mamlaka za soka nchini Misri ikitaka pambano lao dhidi ya Pyramids FC kuchezeswa na marefa wa kigeni.
Mchezo huo wa Egyptian Premier League unatarajiwa kuchezwa Aprili 27, 2026, ukiwa ni moja ya mechi zenye uzito mkubwa katika hatua ya mwisho ya ligi na mbio za ubingwa.
Taarifa kutoka vyanzo mbalimbali vya michezo zinaeleza kuwa uongozi wa Al Ahly umechukua hatua hiyo kufuatia kutoridhishwa na maamuzi ya waamuzi wa ndani katika michezo yao ya hivi karibuni. Klabu hiyo inaamini kuwa matumizi ya marefa wa kigeni yatasaidia kuongeza uwazi na haki katika mchezo huo muhimu.
Si mara ya kwanza kwa mabingwa hao wa kihistoria Afrika kuibua hoja hiyo, kwani katika misimu iliyopita wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa marefa wa kimataifa katika michezo mikubwa, hasa wanapokutana na wapinzani wao wakuu.
Pambano dhidi ya Pyramids linakuja katika kipindi chenye msongamano wa ratiba kwa Al Ahly SC, ambao pia wanatarajiwa kuvaana na Zamalek SC Mei 1, katika mechi nyingine yenye mvuto mkubwa kwa mashabiki wa soka nchini humo.
Kwa mujibu wa kanuni za ligi ya Misri, klabu zinaweza kuomba marefa wa kigeni kwa mechi maalum endapo zitakidhi masharti, ikiwemo kugharamia gharama za usafiri na malazi ya waamuzi hao.
Al Ahly wanashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi wakiwa na alama 44 sawa na Pyramids huku Zamalek wakiongoza ligi wakiwa na alama 46.
Kama Al Ahly itakosa ushindi dhidi ya Pyramids na pia kukosa ushindi dhidi ya Zamalek katika mchezo utakaofuata, watakuwa hatarini kukosa nafasi ya kushiriki michuano ya ligi ya mabingwa (CAFCL) msimu ujao kwani wanaweza wasimalize katika nafasi mbili za juu.



