Kiungo mkongwe wa AC Milan na nahodha wa timu ya taifa ya Croatia, Luka Modric (40), anatarajiwa kukosa mechi zote zilizosalia za msimu wa Serie A baada ya kupata jeraha la shavu katika mchezo dhidi ya Juventus uliochezwa Jumapili ya jana.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo, Modric alipata jeraha hilo baada ya kugongana vichwa na kiungo wa Juventus, Manuel Locatelli, katika dakika za mwisho za mchezo uliomalizika kwa sare tasa ya 0-0.
Baada ya tukio hilo, mchezaji huyo alionekana kuendelea kucheza kwa muda mfupi kabla ya kuondolewa uwanjani kutokana na maumivu makali, huku akiondoka akiwa ameshikilia shavu lake la kushoto. Uchunguzi wa kitabibu uliofanyika baadaye umebaini kuwa amepata fracture ya shavu (cheekbone fracture) inayohitaji upasuaji wa haraka.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa jeraha hilo ni kubwa na litamuweka nje kwa muda wote uliosalia wa msimu wa 2025/26, huku akitarajiwa kufanyiwa upasuaji siku ya Jumatatu.
Licha ya kukosa mechi za klabu, taarifa zinaeleza kuwa Modric anatarajiwa kuwa na matumaini ya kurejea mapema kujiandaa na michuano ya Kombe la Dunia la 2026 akiwa na timu ya taifa ya Croatia.
Madaktari wa timu hiyo wanasema endapo atapona vizuri, huenda akatumia kifaa maalum cha kujikinga usoni (protective mask) wakati wa mashindano hayo.
Kukosekana kwa Modric ni pigo kubwa kwa AC Milan, ambao bado wanapigania nafasi za juu kwenye Serie A na pia mafanikio ya mwisho wa msimu. Kiungo huyo mkongwe amekuwa mhimili muhimu wa safu ya kati kutokana na uzoefu wake mkubwa na uwezo wa kuongoza mchezo.



