Arbeloa, Mbappe katika vita ya maneno Real Madrid

Joel JJ By Joel JJ • 15th May 2026


 Arbeloa, Mbappe katika vita ya maneno Real Madrid

Klabu ya Real Madrid imejikuta katikati ya mjadala mpya baada ya kuibuka kwa mvutano wa maneno kati ya mshambuliaji wake nyota Kylian Mbappé na kocha wake Álvaro Arbeloa, hali inayozidi kuvuta hisia za mashabiki.

Mvutano huo ulianza baada ya Mbappé kuonyesha kutoridhishwa na muda wake wa kucheza katika baadhi ya mechi muhimu Alhamisi usiku akiachwa benchi hadi kipindi cha pili kwenye mchezo dhidi ya Real Oviedo ambao Real Madrid ilishinda mabao 2-0.

Inadaiwa kuwa mshambuliaji huyo alielezea hisia zake kwa kauli iliyozua tafsiri tofauti, akionekana kudokeza kutokubaliana na nafasi yake ndani ya kikosi cha kwanza.

Kwa upande wake, Arbeloa ameripotiwa kujibu kwa msimamo mkali, akisisitiza kuwa maamuzi yote ya kiufundi hufanywa kwa misingi ya nidhamu, utimamu wa wachezaji na mahitaji ya kikosi, si kwa upendeleo binafsi. Ameeleza kuwa kila mchezaji anapaswa kuheshimu mfumo wa benchi la ufundi.

Hali hiyo imezua mjadala mkubwa ndani ya klabu, huku wachambuzi wakionya kuwa migogoro ya aina hiyo inaweza kuathiri utulivu wa chumba cha kubadilishia nguo ikiwa haitashughulikiwa kwa haraka.

Hata hivyo, baadhi ya watu wa karibu na klabu wanaamini kuwa hali hiyo ni sehemu ya ushindani wa kawaida katika klabu kubwa inayobeba matarajio makubwa kama Real Madrid.

Mbappé, ambaye ni miongoni mwa nyota wakuu wa kikosi hicho, bado anachukuliwa kama mhimili muhimu katika safu ya ushambuliaji licha ya kuibuka kundi kubwa la mashabiki ambao wanashinikiza mshambuliaji huyo aondoke.

Wakati akiingia kwenye kipindi cha pili mchezo dhidi ya Oviedo, Mbappé alikumbana na zomea zomea ya mashabiki lakini mwenyewe amesisitiza ni jambo la kawaida kwani mashabiki walikuwa na matarajio makubwa kwao lakini wamewaangusha kwa kushindwa kutwaa taji lolote msimu huu.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.